Mbunge wa Gatundu Kusini aachiliwa kwa dhamana

Martin Mwanje
2 Min Read

Mahakama Kuu ya Machakos imemwachilia kwa dhamana ya shilingi milioni 1 mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe.

Hii ni baada mbunge huyo kukana mashtaka ya mauaji dhidi yake. Alitakiwa pia alipe dhamana mbadala ya shilingi milioni 2 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Kagombe anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mwendeshaji boda boda David Nduati Wataha aliyepigwa risasi mnamo Mei 17, 2024 katika eneo la Kimuchu, mtaa wa Makongeni mjini Thika.

Mwendeshaji boda boda huyo alikumbana na mauti baada ya vurugu kuzuka baina ya wafuasi wa mbunge wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a na Mwakilishi wa Wadi ya Kamenu Peter Mburu, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa soko katika wadi ya Kamenu.

Jaji Francis Olel alikuwa ametoa agizo la Kagombe kufanyiwa uchunguzi wa kiakili wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo  Jumatatu wiki hii.

Mbunge huyo alifanyiwa uchunguzi huo juzi Jumatano kabla ya kesi yake kuendelea.

“Mahakama imezingatia maombi ya upande wa mashtaka na mawakili wa utetezi na hivyo kuamuru mshtakiwa aachiliwe kwa bondi ya shilingi milioni 2 au dhamana ya shilingi milioni 1 pesa taslimu na mdhamini wa kiasi sawa na hicho,” alisema Jaji Olel.

Kesi hiyo itatajwa Julai 17, 2024.

Jaji Olel alionya mshukiwa dhidi ya kuwasiliana na mashahidi wala kuzuru eneo la tukio.

“Mshukiwa hapaswi kuwasiliana na mashahidi wala kuzuru eneo ambalo kisa hicho kilitokea,” Olel aliamuru.

Ombi kutoka kwa mawakili wa Kagombe la kutaka kesi hiyo kuhamishiwa katika mahakama za Milimani, Thika au Kiambu lilikataliwa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *