Wanasiasa wahimizwa kukomesha matamshi yasiyofaa kuhusu uenyekiti wa tume ya AU

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi amewataka wanasiasa kukoma kutoa matamshi ambayo hayafai na ambayo huenda yakahujumu uwaniaji wa Kenya wa uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika AU.

Musalia ambaye pia ni waziri wa masuala ya nchi za nje, anasema wanasiasa wanafaa kuchukulia suala hilo kwa uzito unaostahili na kutanguliza maslahi ya nchi katika uwaniaji wa wadhifa huo.

Kulingana na waziri huyo, hatua ya kutafuta wadhifa huo wa bara Afrika sio njia ya kutafutia mtu mmoja kazi kama zawadi ila wakenya wanafaa kufikiria kuhusu maslahi ya nchi nzima.

Aliwahimiza wanasiasa kutoambatanisha uwaniaji wa wadhifa huo na Raila Odinga lakini wafahamu kwamba ni nchi ya Kenya inapendekeza Raila kama mwaniaji ili aweze kutoa huduma ya uongozi.

“Kenya inatafuta njia za kusaidia kuleta umoja barani Afrika na kutatua changamoto ambazo zinakumba mataifa ya bara hili.” alisema Mudavadi akiongeza kwamba Rais Ruto alimchagua Raila kuwania wadhifa huo kwa sababu ya tajriba yake ambayo itasaidia Afrika kupata suluhisho kwa changamoto zake.

Mudavadi alikuwa akizungumza kwenye mazishi ya Henry Chakava huko Vokoli, eeneo bunge la Sabatia kaunti ya Vihiga.

Alimsifia marehemu Chakava mwanzilishi wa kampuni ya uchapishaji wa vitabu ya “East African Education Publishers” ambaye alisema atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya uchapishaji na ya elimu kwa jumla.

Share This Article