Gavana wa kaunti ya Kisii Paul Simba Arati ameteua Naibu Gavana mpya siku chache tu baada ya aliyekuwa naibu wake Dkt. Robert Monda kuondolewa afisini na bunge la Seneti.
Arati amemchagua Elijah Obebo ambaye kwa sasa anahudumu kama mwenyekiti wa bodi ya utumishi wa umma ya kaunti ya Kisii. Haya yanajiri wakati ambapo Dkt. Monda amekimbilia mahakama kupinga kuondolewa kwake afisini.
Dkt. Monda anatuhumiwa na bunge la kaunti ya Kisii kwa kukiuka katiba, matumizi mabaya ya mamlaka, utovu wa nidhamu na makosa mengine chini ya sheria za kitaifa, makosa ambayo yalithibitishwa na bunge la Seneti.
Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Phillip Nyanumba alisema leo kwamba Arati amemteua Obebo kwa wadhifa wa Naibu Gavana na atasailiwa na kuidhinishwa au kukataliwa na bunge hilo.