Kenya imeandaa mkutano wa saba wa Tume ya Ushirikiano wa Pamoja na Misri.
Mkutano huo uliofanyika jijini Nairobi jana Alhamisi ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi na mwenzake wa Msiri Sameh Shoukry.
Mudavadi anasema ulitoa fursa muhimu ya kutathmini mafanikio ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili na hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa ili kuboresha uhusiano huo.
“Majadiliano yaliangazia kujitolea kwetu kwa pamoja kuimarisha ushirikiano na nyanja mbalimbali za maslahi ya pande mbili,” alisema Mudavadi baada ya mkutano huo.
“Wakati wa mkutano, makubaliano ya pande tatu yalitiwa saini ili kuboresha ushirikiano katika huduma za utabibu wa mifugo, masuala ya baharini, na nishati mbadala.”
Mudavadi alisema Kenya bado imedhamiria kuunga mkono na kuzikaribisha kampuni za Misri ili kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Misri ni miongoni mwa nchi vinara zinazofanya biashara na Kenya barani Afrika na inaongoza katika uagizaji wa majani chai kutoka Kenya.