Zaidi ya wanafunzi 500 wa shule za upili na vyuo vya kadri katika kaunti ya Murang’a wamepokea ufadhili wa basari shilingi milioni 5 kutoka kwa mwakilishi wa kike Betty Maina.
Akizungumza katika uwanja wa Kimorori eneo la Kenol siku ya Jumanne, mwakilishi huyo wa kaunti ya Murang’a bungeni alisema ofisi yake imejitolea kuhakikisha kuwa wanafunzi wote kutoka familia zisizojiweza wanapata fursa ya kusoma kama wanafunzi wengine.
“Leo wanafunzi 506 wa vyuo, vyuo vya elimu ya juu na sekondari, wakiwemo wenye ulemavu wanapokea jumla ya Sh milioni 5.2 kugharamia masomo yao,” alisema Maina.
“Elimu ni ufunguo ambao utawasaidia kufungua milango yote ya fursa zinazopatikana kwao,” aliongeza.
Maina alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa fedha za matumizi ya shule zimetolewa kwa wakati.
“Tumeshuhudia serikali ikitoa asilimia fulani kwa muhula wa shule na inazuia asilimia nyingine,
Muhula unaofuata wanatoa kiasi fulani kwa muhula huo bila kufuta ruzuku ya wanafunzi ya muhula uliopita, ambayo inaishia kuwa mzigo kwa wakuu wa shule ambao wanapaswa kuendesha shule” alisema Maina.