Naibu Rais Rigathi Gachagua amewahakikishia wamiliki wa ardhi katika kijiji cha Maina, mjini Nyahururu, eneo bunge la Laikipia Magharibi kuwa serikali inakusudia kuwapatia hatimiliki za ardhi katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Akizungumza wakati akiwahutubia wakazi hao jana Jumatatu, Gachagua alisema serikali ya Rais William Ruto inadhamiria kuhakikisha wakazi hao wamailiki kikamilifu ardhi yao na kufaidika kutokana nayo.
“Tunafanyia kazi hatimiliki za wakazi hapa katika kijiji cha Maina kwa sababu wamaekuwa wakiziulizia kwa muda mrefu. Tunataka kuhakikisha mnapata hatimiliki zenu katika kipindi cha miezi sita ijayo,” alisema Naibu Rais alipotangamana na wakazi hao wakati wa ziara yake ya maendeleo katika eneo hilo.
Mbali na kukabidhiwa hatimiliki hizo muhimu, Gachagua alisema barabara za eneo hilo pia zitawekwa lami ili kukifungua kijiji hicho.
Kadhalika alisema serikali inashughulikia mizozo kati ya binadamu na wanyama pori katika eneo hilo ili kuepusha madhara zaidi kwa wakazi.
“Tunataka watu wafurahie matunda ya jasho lao mashambani mwao bila uoga wa kupoteza uwekezaji wao kwa wanyama pori hapa,” alisema Gachagua.
Aliyasema hayo akiwa ameandamana na Gavana wa Laikipia Joshua Irungu, Naibu Gavana Rueben Kamuri na Seneta wa Laikipia John Kinyua miongoni mwa viongozi wengine.