Ruto afungua rasmi kongamano la uwekezaji Homa Bay

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto leo Jumanne alijiunga na viongozi mbalimbali wanaohudhuria kongamano la kimataifa la uwekezaji la kaunti ya Homa Bay, kongamano ambalo alifungua rasmi.

Akihutubia washiriki, kiongozi wa nchi alimmiminia sifa gavana wa kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga akisema amedhihirisha uongozi wa kipekee.

Rais alisema Wanga ndiye gavana wa kwanza kabisa nchini kushirikiana na serikali ya kitaifa katika utekelezaji wa mpango wa nyumba za bei nafuu.

Aliongeza kwamba Wanga ni kati ya magavana watatu ambao wametuma maombi ya kupatiwa leseni ya kujenga eneo spesheli la kiviwanda nchini na kufanikiwa.

Rais Ruto alimshukuru Gavana huyo kwa kuwa mfano mwema wa ushirikiano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti katika mradi wa nyumba za gharama nafuu.

Kongamano la kimataifa la uwekezaji la kaunti ya Homa Bay limeanza rasmi leo Jumanne na litaendelea kwa siku tatu kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa Kenya na wa nchi nyingine kutumia fursa za uwekezaji zilizopo kwenye kaunti hiyo.

Website |  + posts
Share This Article