Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale amelaani shambulizi la wanamgambo wa Al-Shabaab katika kambi moja ya wanajeshi jijini Mogadishu nchini Somalia.
Wanajeshi watatu wa Umoja wa Milki za Kiarabu, UAE na mmoja wa Bahrain waliangamia kwenye shambulizi hilo.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Duale alitoa taarifa akisema anasimama na serikali za Somalia na UAE kulaani kitendo hicho alichokitaka kuwa cha uwoga.
Jumamosi, Februari 10, 2024, wanamgambo wa Al-Shabaab walishambulia kambi ya wanajeshi ya General Gordon inayosimamiwa na UAE mjini Mogadishu nchini Somalia.
Duale alipongeza juhudi za wanajeshi wajasiri walioangamia akielezea imani kwamba watu wa UAE watapona kutokana na shambulizi hilo na kuendeleza juhudi za kukabiliana na ugaidi.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ametoa salamu za rambirambi kwa UAE kwa kupoteza wanajeshi wake kwenye shambulizi la magaidi.
Miili yao tayari imesafirishwa kuelekea UAE kwa ajili ya heshima za mwisho na mazishi.
Taarifa zaidi zinaashiria kwamba mmoja wa wanajeshi hao alikuwa na majeraha mabaya na alikata roho akiwa kwenye safari hiyo ya kurejea UAE.
Kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab limekuwa likiendeleza mashambulizi nchini Somalia na katika nchi nyingine zilizo karibu huku Umoja wa Afrika nao ukiendeleza makabiliano dhidi ya kundi hilo.