Waziri wa Utalii Daktari Alfred Mutua amezindua mpango wa kuhamisha vifaru weusi 21 kutoka mbuga za wanyama za Nairobi, Ol Pejeta na Lewa hadi mbuga ya Loisaba.
Waziri Mutua alifafanua kwamba wanatekeleza awamu ya 7 ya mpango wa kurejesha vifaru weusi nchini Kenya kwa ushirikiano na wadau wengine.
Huku akitaja mpango huo kuwa unaowiana na sheria ya kutunza wanyamapori, Daktari Mutua alisema lengo lao ni kupunguza idadi ya vifaru hao weusi kutoka maeneo ambako ni wengi ili kuhakikisha ukuaji endelevu wa wanyama hao.
Aliongeza kuwa idadi ya vifaru weusi imeongezeka katika muda wa miaka 30 iliyopita kutoka 384 hadi 1,000, nusu ya idadi wanayotarajia kuafikia kufikia mwaka 2037 ya vifaru 2,000.
Kenya imeorodheshwa nambari 3 ulimwenguni baada ya Afrika Kusini na Namibia katika idadi ya wanyama hao.
Mpango wa urejesho wa vifaru nchini Kenya unalenga pia vifaru weupe wa kusini na wa kaskazini kupitia mpango wa BioRescue.
Waziri Mutua anasisitiza kwamba juhudi za kuzuia uwindaji haramu ni lazima ziimarishwe, hata ingawa tumefanikiwa kuukomesha, kufuatia ongezeko lake katika nchi za Kusini mwa Afrika.
“Serikali kupitia kwa wizara ya utalii imejitolea kuhakikisha uwepo wa rasilimali zinazohitajika katika utunzaji wa Vifaru,” alisema Mutua kupitia taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mpango wa kuhamisha vifaru hao ulizinduliwa katika mbuga ya wanyama ya Nairobi.