Mabingwa watetezi Senegal wameanza vyema harakati za kuwania kombe la AFCON nchini Ivory Coast, baada ya kuwakanyaga The Scorpion kutoka Gambia mabao matatu kwa bila .
Mchuano huo umesakatwa Jumatatu jioni katika uga wa Charles Konan Banny Stadium mjini Yamoussoukro.
Mchecheto wa Gambia ambao wanaorodheshwa wa mwisho katika kipute cha mwaka huu, ulisababisha makosa kwenye safu ya nyuma na kumpa Sadio Mane fursa ya kutoa pasi kwa Pape Gueye aliyetikisa nyavu kunako dakika ya 4.
Juhudi za limbukeni Gambia kurejea mchezoni zilidumazwa baada ya kiungo Ebou Adams kupigwa kadi ya umeme mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Teranga Lions walirejea kipindi cha pili roho juu ndiposa kiungo Lamine Camara akatanua uongozi kunako dakika ya 52 akiunganisha mkwaju wa Ismail Sarr.
Barubaru Camara alifyatua tobwe la dakika 86, akiunganisha mkwaju wa Illiman Ndiaye dakika 86 na kuhitimisha kibarua kwa Senegal kwa goli la tatu.