Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ametoa wito kwa kanisa kuwa nguzo muhimu katika kukuza amani nchini na kuunga mkono mpango wa serikali wa kuwaunganisha Wakenya.
Mudavadi amesema kanisa hutekeleza wajibu muhimu katika jamii na linapaswa kuwa kioo cha nchi katika mantiki ya uthabiti na ustawi katika nyanja zote za maisha.
Alitoa kauli hizo, wakati pia akiwatahadharisha Wakenya dhidi ya manabii wa uongo wanaongezeka, ambapo watu wengi wasiokuwa na hatia wamejipata wakilaghaiwa.
Mudavadi alisema manabii wa uongo wamesababisha maangamizi nchini na kimataifa.
“Watu wasiokuwa na hatia wamesalimisha afya na mali yao kwa watu ambao hawajafanya chochote kuwasaidia kupata mali. Haileti mantiki wakati mtu kama profesa ama daktari au mtu aliyeelimika anasalimisha mali yake aliyotafuta kwa miaka mingi, kuiacha familia yake na kumfuata nabii wa uongo ambaye kamwe hajawahi tia guu katika darasa la kwanza,” alisikitika Mudavadi.
Alitoa wito kwa kanisa kuisaidia serikali kutambua wachungaji matapeli na kuwawajibisha kwani wanaliharibia kanisa sifa.
Mudavadi alitoa kauli hizo wakati wa Mkutano wa Dunia wa Mwaka 2023 wa Kanisa la Friends Church (Quakers) unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Kabarak mjini Nakuru.
Kauli zake zinawadia wakati ambapo wachungaji wenye mienendo ya kutilia shaka wameibuka nchini huku matukio katika msitu wa Shakahola yakiwaacha wengi vinywa wazi kote duniani.
Katika msitu huo uliopo katika kaunti ya Kilifi, miili zaidi ya 300 ya wafuasi wanaominika kuwa wa dhehebu la mchungaji Paul Mackenzie imefukuliwa na zoezi la ufukuaji bado halijakamilika.
Kutokana na hali katika msitu huo, serikali imeapa kukabiliana vikali na wachungaji matapeli nchini.