Ghasia zinaendelea kushuhudiwa nchini Ufaransa kwa siku ya nne mfululizo, licha ya kuwepo kwa maafisa wengi wa polisi.
Magari na majengo yaliteketezwa, mabohari kuporwa na takriban watu 900 kutiwa mbaroni, huku familia na marafiki wakijiandaa kumzika kijana mwenye umri wa miaka 17, aliyeuawa na polisi nchini humo tukio ambalo lilichochea ghasia hizo.
Serikali ya Ufaransa imesema ghasia hizo zilianza kusitishwa kutokana na usalama ulioimarishwa, japo tayari uharibifu ulikuwa umetekelezwa.
Kulingana na wizara ya usalama nchini humo, watu 994 walikuwa wamekamatwa kufikia Jumamosi asubuhi.
Takriban maafisa wa polisi 45,000 waliojihami kwa magari ya kivita, walianza shughuli ya kurejesha amani siku ya Ijumaa, huku uporaji na ghasia zikiripotiwa katika majiji ya Lyon, Marseille na Grenoble ambako magenge ya vijana yalikuwa yakipora maduka na kupambana na maafisa hao wa polisi.