Mapato ya serikali kupitia eCitizen yazidi milioni 900 kwa siku

Marion Bosire
2 Min Read

Kwa mara ya kwanza, mapato ambayo serikali inakusanya kupitia mtandao wa eCitizen kwa siku yamepita shilingi milioni 900.

Katibu wa huduma za uhamiaji na nyingine kwa wananchi Julius Bitok anasema kwamba takwimu zinaonyesha kwamba shilingi milioni 903.6 zilikusanywa kwenye mtandao huo Jumatano, Disemba 20, 2023.

Kulingana naye, thuluthi moja ya pesa hizo ambazo watu walilipia huduma mbali mbali za serikali, zililipwa kwa kutumia sarafu ya Dola.

Kiwango hicho cha mapato ambacho kinazidi kuongezeka kinatokana na agizo la Rais William Ruto kwa mashirika yote ya serikali kuweka huduma zao kwenye mtando wa eCitizen, kufikia mwisho wa mwaka huu.

Malipo yote pia aliagiza yafanywe kupitia kwa nambari ya Paybill ya 222222 kwa lengo la kuhimiza uwazi na usimamizi bora wa pesa za serikali.

Ongezeko la mapato ya kila siku kwa shilingi milioni 300 ikilinganishwa na mwezi uliopita yanatokana na hatua ya huduma zipatazo elfu 14 za serikali kuwekwa kwenye mtandao.

Takwimu za wizara ya fedha zinaonyesha kwamba pesa zilizokusanywa mwezi Novemba zilikuwa bilioni 4.664 huku mapato ya mwezi Juni mwaka huu kabla ya agizo la Rais, yakiwa bilioni 1.44.

Mapato ya miezi ya Julai, Agosti na Septemba ni shilingi bilioni 2.362, 3.636 na 4.233 mtawalia.

Serikali inategemea ongezeko la wakenya 5000 wanaotumia mtandao wa eCitizen kila siku kuongeza mapato yake.

Watumizi waliopo kwenye mtandao huo ni milioni 11 na huenda wakaongezeka kulingana na ongezeko la huduma kwenye mtandao wa eCitizen.

Share This Article