Rais William Ruto ametangaza habari njema kwa wabunifu na wale ambao huwaza na kuandaa video kwenye mitandao ya Facebook na Instagram.
Kwenye hotuba yake ya sikukuu ya Jamhuri leo, kiongozi wa nchi alisema kwamba jana kampuni ya Meta inayomiliki mitandao hiyo ilijitolea kusaidia waandaaji wa video hizo ili waweze kujipatia pesa.
Kulingana naye Meta inapanga kuongeza idadi ya watu wanaolipwa kufuatia vitu ambavyo wanachapisha humo.
Alisema kwamba katika sherehe sawia mwaka jana aliahidi kwamba angebadilisha sekta ya ubunifu na michezo ili iweze kuwa kitega uchumi kwa wengi na kwa sababu hiyo walizindua mpango wa Talanta Hela mwezi Juni mwaka huu.
“Wanamichezo wetu wanaendelea kuletea nchi yetu fahari. Timu yetu ya wanawake ya mpira wa voliboli na timu ya wanaume ya mchezo wa raga zimefuzu kwa michezo ya Olimpiki mwaka 2024 jijini Paris.” alisema Rais.
Serikali yake alisema inaendelea kuchukua hatua za kimakusudi kujenga na kuwekeza zaidi katika uchumi wa ubunifu akitaja ushirikiano uliopo kati ya Kenya na waandalizi wa tuzo za muziki za Grammy.
Alizungumzia pia mipango iliyopo ya waandalizi wa filamu kutoka Hollywood ya kuja kuandaa filamu nchini Kenya mwakani.
Kampuni ya Google pia kwa ushirikiano na wizara za elimu na mawasiliano na uchumi dijitali inapanga kuanzisha mafunzo maalum ya kusimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari chini ya mtaala ulioidhinishwa na taasisi ya mitaala nchini KICD.
Alisema mpango huo unaolenga wanafunzi milioni 4 utahitaji walimu elfu 42.