Rais William Ruto amesema kupatikana kwa huduma za serikali kupitia kwa mfumo wa digitali wa e-Citizen kutahakikisha Wakenya wanapata huduma bora bila mahangaiko.
“Hauhitaji kumfahamu yeyote, kutembelea ofisi yoyote, kumshawishi mtu yeyote wala kutoa hongo ili kuhudumiwa,” alisema Rais Ruto wakati wa uzinduzi wa programu ya Gava Mkononi leo Ijumaa.
“e-Citizen itaboresha utoaji huduma na uwajibikaji serikalini.”
Utoaji wa leseni za kuendesha gari, usajili wa biashara, hati ya maadili kutoka kwa huduma ya polisi, usajili wa hati za ndoa na huduma za uhamiaji ni miongoni mwa huduma zilizowekwa kwenye mfumo wa e-Citizen zitakazopatikana kupitia kwa programu ya Gava Mkononi.
Huduma 5,000 za serikali zimewekwa kwenye mfumo huo na serikali inalenga kuweka takriban huduma zote 10,000 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Uzinduzi wa programu ya Gava Mkononi unakuja wakati Wakenya wengi sasa wana simu za mkononi aina Smartphones na hivyo kurahisisha utumiaji wake.
Wakati wa sherehe za sikukuu ya Jamhuri mwaka 2022, Rais Ruto aliahidi kuwa huduma 5,000 za serikali zitapatikana kupitia mfumo wa e-Citizen ili kurahisisha utoaji huduma, ukusanyaji wa mapato, kuimarisha uwazi na kutokomeza ufisadi.
Kufikia mwezi Januari mwaka huu, kulikuwa na huduma mpya 391 katika mfumo wa e-Citizen.