Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu siku ya Jumamosi ametangaza kuwa wizara yake imetoa shilingi bilioni 3.9 katika awamu ya kwanza ya kugharimia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu vya umma, wanaofadhiliwa na serikali chini ya mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu.
Kulingana na waziri huyo, wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo ni wale waliofaulu kutuma maombi yao kupitia tovuti ya ufadhili wa elimu ya juu.
Waziri Machogu alisema, takriban wanafunzi 115,892 wa mwaka wa kwanza, walifanikiwa kutuma maombi hayo kufikia Novemba 29 mwaka huu.
Alisema hazina ya vyuo vikuu itasambaza shilingi bilioni 3.9 moja kwa moja kwenye vyuo vikuu, ili fedha hizo zigharimie karo za wanafunzi waliofaulu kutuma maombi yao chini ya mfumo huo mpya.
Machogu alisema, vyuo vikuu vyote vitapokea fedha za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wao, ifikapo tarehe nne mwezi huu.
Mapema mwezi huu, serikali kupitia bodi ya mikopo ya elimu ya juu, ilitoa shilingi bilioni 5.3 zikiwa ni za mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza.