Msimamizi wa ADC aonywa kwa kutofika bungeni

Marion Bosire
2 Min Read
Mheshimiwa Emmanuel Wangwe

Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya uwekezaji katika usimamizi wa huduma za jamii na kilimo Emanuel Wangwe ametoa onyo kali kwa kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika la maendeleo ya kilimo nchini, ADC Mohammed Bule kwa kukosa kufika bungeni leo.

Bule ambaye alistahili kufika mbele ya kamati hiyo kama shahidi kujibu maswali ya uchunguzi wa matumizi ya pesa katika shirika hilo la ADC kulingana na ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, anasemekana kuwa nchini Uganda kwa ziara ya kikazi.

Msamaha aliotuma Bule wa maneno kupitia kwa mkurugenzi anayehusika na mipango katika ADC Winnie Macharia, haukumfurahisha Wangwe.

Shahidi anayealikwa na kamati ya bunge anahitajika kuomba msamaha wa kukosa kufika kabla ya siku ya kikao na kupitia barua na wala sio maneno matupu.

Wangwe alimtaja Macharia kuwa mgeni asiyefahamika na kamati hiyo huku akisema hawawezi kukubali msamaha wa maneno kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa shirika kubwa kama ADC.

Kutokana na hilo, Macharia na wengine aliokuwa ameandamana nao walifukuzwa na kamati hiyo.

Walitumwa wamjuze Bule kwamba kamati hiyo iko tayari kuainisha maswali yaliyoibuliwa kuhusu shirika la ADC faraghani.

Bule sasa anahitajika kuomba msamaha rasmi kwa kudharau kamati hiyo ya bunge.

Wangwe, amempa Bule tarehe nyingine ya kufika mbele ya kamati ambayo ni Novemba 29, 2023.

Website |  + posts
Share This Article