Watu 24 wameuawa katika mashambulizi ya mabomu yanayotekelezwa na Marekani nchini Yemen.
Rais Donald Trump wa Marekani aliagiza na kutangaza mashambulizi ya kiwango cha juu dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen bada ya kundi hilo kutoa vitisho dhidi ya Israel.
Wa-Houthi hao walikuwa wametishia kurejelea mashambulizi ya meli zinazohusishwa na Israel katika bahari ya shamu kutokana na hatua ta Israel ya kudhibiti Gaza.
Mashambulizi hayo ya Marekani yaliyoanza jana Jumamosi yameendelea hadi leo Jumapili na yamesababisha vifo vya watu 23 katika jiji kuu Sanaa na katika mkoa wa kaskazini wa Saada.
Hayo ni kulingana na runinga ya Al Masirah, iliyoripoti kwamba wahasiriwa wa Saada walijumuisha watoto wanne na mwanamke mmoja na majeruhi 22.
Mashambulizi haya ya Marekani juu ya Yemen ndiyo hatua kuu ya kijeshi ya Marekani tangu Trump aliporejea katika uongozi wa taifa hilo.
Trump alitumia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kuwasilisha onyo dhidi ya waasi wa Houthi ambapo alisema kwamba wasipokomesha mashambulizi, watafikwa na mambo ambayo hawajawahi kuona.
“Nimeagiza jeshi la Marekani leo lianzishe mashambulizi makali dhidi ya magaidi wa Houthi nchini Yemen.” Alisema Trump.
Kiongozi huyo alitoa pia ujumbe kwa Iran akiitaka ikomeshe mara moja usaidizi inaotoa kwa kundi la Houthi. Alisema Marekani itawajibisha Iran iwapo itashambulia Marekani na halitakuwa jambo zuri.
Kundi la Houthi ambalo linadhibiti eneo kubwa la nchi ya Yemen halijashambulia meli yoyote hata baada ya kutishia kufanya hivyo wiki moja iliyopita.
Vitisho hivyo vilitokana na hatua ya Israel ya kudhibiti chakula, mafuta na bidhaa nyingine muhimu katika ukanda wa Gaza.
Msemaji wa Houthi Mohammed Abdul-Salam alilaumu Marekani kwa kulifanya suala la vitisho hivyo kuwa kubwa kwa lengo la kuvutia hisia za umma.