Wakfu wa mkewe naibu rais wapokea ufadhili kutoka KPC

Marion Bosire
1 Min Read

Mipango ya kijamii inayolenga watu wanaoishi katika mazingira magumu inayoongozwa na mkewe naibu rais Rigathi Gachagua mchungaji Dorcas Rigathi imepigwa jeki kwa shilingi milioni 3 kutoka kwa wakfu wa kampuni ya mabomba nchini Kenya Pipeline.

Dorcas huendesha mipango kadhaa ya kusaidia jamii chini ya wakfu wake “Dorcas Rigathi Foundation – DRF”

Mkurugenzi mkuu wa Kenya Pipeline Joe Sang aliwasilisha hundi ya pesa hizo kwa mchungaji Dorcas Rigathi katika makazi yake rasmi huko Karen leo.

Sang alisema kwamba wakfu wa KPC umekuwa ukiendesha mipango mbali mbali kwa miaka mingi kama kusaidia watoto walemavu kupata elimu kama namna ya kutekeleza jukumu la kampuni hiyo kwa jamii.

Alisifia maono ya afisi ya mke wa naibu rais ambayo yanalenga walio katika mazingira magumu kama vile mtoto wa kiume.

Mchungaji Dorcas Rigathi, kwa upande wake alishukuru wakfu wa KPC kwa ukarimu akisema mchango wao utawekezwa katika kuhakikisha familia na jamii zilizostawi.

Alitoa hakikisho kuhusu kujitolea kwake katika kuwezesha, kushauri na kuwianisha vijana na ndoto zao na hatima maishani ili Kenya iwe na familia imara.

Share This Article