Wafanyabiashara wawili wa eneo la Cheptulu katika kaunti ya Vihiga wanaomba waziri wa usalama wa taifa Profesa Kithure Kindiki aingilie kati na kuhakikisha wanapata haki.
Wawili hao Irene Jemutai na kakake Peter Kiplimo wanadai kushambuliwa na maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Cheptulu na kupokonywa pesa na simu za rununu.
Irene anamiliki duka katika eneo hilo anasema alipigiwa simu na watu asiowajua waliomtaka afike kwenye afisi za taasisi ya kifedha ambayo anasema ni bandia na maelekezo waliyompa yangemfikisha kwenye msitu.
Baada ya kukatiza mawasiliano na watu hao, Irene anasema watu waliokuwa wamevaa mavazi ya raia walifika kwenye duka lake kwanza wakajisingizia kuwa wateja na baadaye maafisa wa polisi.
Walichukua simu zake na kumwagiza afunge duka aandamane nao Hadi kituo cha polisi kilicho karibu. Alipoona kwamba gari walilokuwa wakitumia halikuwa na polisi alipiga mayowe na wakazi wa eneo hilo wakakusanyika.
Kakake naye alikuwa amefika eneo hilo akitaka kujua ni kwa nini dadake alikuwa anachukuliwa. Anasema watu hao walifyatua risasi hewani kutawanya umati kisha wakaondoka na Irene na kakake.
Kiplimo anadai kupokonywa simu na shilingi laki 1 kituoni humo.
Dakika chache baadaye alirudishiwa simu bila pesa na kuambiwa aondoke na dadake kwani mhalifu aliyekuwa akitafutwa ameshapatikana.
Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu na familia ya waathiriwa wanataka Waziri wa usalama wa ndani aingilie kati na kuchunguza maafisa wake ili kulinda wakenya wote na mali yao bila ubaguzi.
Kamanda wa polisi wa Hamisi Bi Ruth Langat amesema uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichotekea.