Wizara ya Sheria ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), imeahidi kutoa dola milioni 5 kwa yeyote atakayesaidia kumkamata Corneille Nangaa ambaye ni kiongozi wa muungano wa mto Kongo, Bertrand Bisimwa na Sultani Makenga ambao ni viongozi wa kisiasa na kijeshi wa vuguvugu la Machi 23 (M23).
Mzozo unazidi kutokota mashariki mwa DRC, huku makundi ya wapiganaji, wakiwemo wale wa M23 wakikbiliana vikali na wanajeshi wa nchi hiyo.
Hadi kufikia sasa, kundi la M23 limetwaa mji wa Goma ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini DRC.
Watu wengine wawili wanaosakwa na serikali ya Felix Tsishekedi, ni waandishi wa habari wanaoishi uhamishoni, huku zawadi ya dola milioni 4 zikitolewa kwa atakayewakamata.
Viongozi hao wa waasi walishtakiwa bila ya kuwepo mahakamani, na kuhukumiwa adhabu ya kifo mwezi Agosti mwaka 2024 na mahakama ya kijeshi mjini Kinshasa kwa uhalifu wa kivita, na kusababisha uasi na uhaini.
Maelfu ya wakazi mashariki mwa DRc wametoroka makwao, wengi wao wakiingia nchi jirani ya Burundi.