Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula amempongeza Rais William Ruto kwa kile alichokitaja kuwa ajenda ya maendeleo yenye mageuzi makubwa katika Kaunti ya Bungoma na eneo lote la Magharibi mwa Kenya.
Wetangula alikuwa akizungumza baada ya kuandamana na ujumbe wa viongozi wa kidini na viongozi waliochaguliwa kutoka Kaunti ya Bungoma hadi Ikulu ya Nairobi.
Alisema mkutano huo ulijikita katika miradi muhimu inayolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hilo. Ujumbe huo uliongozwa na Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka.
Miongoni mwa miradi mikuu iliyojadiliwa ni upanuzi uliopangwa wa Reli ya Kisasa hadi Malaba kupitia Miyanga, kuanzishwa kwa mji wa kisasa huko Bungoma, ufufuzi wa sekta ya sukari, na mradi uliopendekezwa wa kuzalisha megawati 45 za umeme kutokana na maji huko Webuye.
Wetang’ula pia aliwapongeza viongozi wa kidini kwa kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa kijamii, akiwataja kama washirika muhimu katika kujenga jamii yenye utulivu.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuchukua vitambulisho vyao vya kitaifa na kujisajili kama wapiga kura kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kuimarisha demokrasia.
Spika huyo pia alimshukuru Rais Ruto kwa kuwateua watu kadhaa kutoka Bungoma katika nyadhifa za juu serikalini, huku akiwataka wakazi kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya serikali.
Rais Ruto kwa upande wake alisema, “Tumefaulu kuimarisha uchumi wetu na kuweka msingi wa mageuzi kutokana na maamuzi ya kijasiri ambayo tumefanya”.
Kiongozi wa nchi alisisitiza kwamba uongozi sio kufurahisha watu kwa maneno matamu, bali unahusu kufanya maamuzi sahihi.