Rais William Ruto ameteua Baraza la watu saba la Uongozi wa Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu (NIF).
Baraza hilo litaongozwa na Waziri wa Fedha John Mbadi na litahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Wanachama wa baraza hilo watakaoiwakilisha serikali wanajumuisha Gavana wa Benki Kuu Dkt. Kamau Thugge na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor.
Wanachama huru wanajumuisha Prof. Benedict Oramah ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Export Development for Africa (FEDA) na Africa Medical Centre for Excellence (AMCE), Faith Boinett ambaye ni mwanasheria wa mahakama kuu na mwenyekiti wa kampuni ya Kenya Pipeline na Paul Russo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Group PLC.
Ricard Etemesi ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya Liberty Holdings Limited ni mwanachama mwingine huru aliyeteuliwa kwenye baraza hilo.
Kwenye taarifa, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema kipaumbele cha baraza hilo kitakuwa kusimamia usajili wa Wakurugenzi wa Bodi ya NIF. Kisha bodi hiyo nayo itakabidhiwa jukumu la kusajili mkurugenzi mtendaji atakayeongoza utekelezaji wa hazina hiyo.
Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu inakusudia kutafuta fedha za kufadhili miradi muhimu nchini kama vile barabara na reli katika azma ya kuhakikisha Kenya inaungana na jumuiya ya mataifa yaliyostawi zaidi duniani.