Kilimo katika kaunti ya Homa Bay kimeimarishwa baada ya mradi wa wafadhili kuanzishwa ambao unalenga kuimarisha ustahimilivu wa hali ya hewa katika uzalishaji wa mazao.
Akizungumza ofisini mwake siku ya Jumanne alipopokea wanadiplomasia wakiongozwa na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Kenya Henriette Geiger, gavana wa Homa Bay Gladys Wanga alisema kuwa mpango huo umewezeshwa kupitia ufadhili wa EU kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti.
Mpango huo unahusisha uzalishaji wa kilimo ambao unapunguza utoaji wa kaboni kwenye anga kupitia matumizi ya mbolea za kikaboni.
Gavana huyo alisema kuwa zaidi ya wakulima 3000 tayari wamepokea vifaa vya kilimo vikiwemo mbegu na mbolea.
Wanufaika watapata vifaa vya kilimo kwa bei nafuu ambapo watalipa asilimia kumi ya gharama zote. Vifaa hivyo vinajumuisha mbegu za mahindi, maharagwe na mawele pamoja na mbolea. Wakulima wa kwanza kunufaika wanatoka kaunti ndogo za Ndhiwa na Karachuonyo.
Wanga alisema kuwa zaidi ya wakulima 6000 wamepata mafunzo kuhusu mbinu za kilimo zinazostahimili hali ya hewa kupitia mpango huo.
Naibu gavana Oyugi Magwanga alisema kuwa mpango huo utawapa moyo wakulima kujihusisha na uzalishsji wa chakula katika kaunti hiyo kutokana na urahisishaji wa kilimo kupitia teknolojia ya kisasa.
“Tunashukuru kama kaunti kwamba zaidi ya wakulima 3000 watafaidika na mbegu na mbolea huku wengine 6000 wakinufaika na uwezeshaji wa kilimo kinachozingatia hali ya hewa,” Magwanga alisema.
Geiger aliwahimiza wakulima kutumia mpango huo kubadilisha maisha yao.
“EU inapanda mbegu ndani yenu lakini ni juu yenu kutumia mbegu hizo na kuzifanya ziwe na faida kwa njia ambayo inaweza kubadilisha maisha yenu,” Geiger alisema.
Alisema kuwa EU imejitolea kukuza uchumi wa kijani kupitia mazoea ya kilimo yanayostahimili hali ya hewa.