Wakenya ughaibuni wahimizwa kuzingatia sheria za nchi husika

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje kadhalika amewataka kuwa na nidhamu na kuwakilisha taswira ya Kenya.

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi akiwa nchini Urusi.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametoa wito kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni kufuata sheria za nchi husika.

Akizungumza Jumanne aliposhiriki mkutano na raia wa Kenya wanaoishi nchini Urusi, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje kadhalika amewataka kuwa na nidhamu na kuwakilisha taswira ya Kenya.

Kwenye mkutano huo, Mudavadi aliwafahamisha Wakenya hao kwamba ziara yake nchini Urusi ililenga kuimarisha zaidi ushusiano kati ya nchi hizo mbili ambao umedumu kwa miaka 60.

Aidha, aliwahakikishia kwamba serikali ya Kenya na Urusi  zimejadiliana na kukubaliana kusitisha kuajiriwa kwa raia wa Kenya kwenye vikosi vya ulinzi vya Urusi.

Aliwakumbusha Wakenya wanaoishi ughaibuni kuwa mabalozi wa taifa hili.

Mudavadi yuko katika ziara rasmi ya kiserikali nchini Urusi, itakayokamilika Machi 18, 2026.

Share This Article