Utawala wa Rais Donald Trump nchini Marekani umechukua hatua ya kuwafuta kazi wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) huku wengine wakipatiwa likizo ya lazima.
Katika ilani iliyopachikwa kwenye tovuti ya USAID, wafanyakazi wote wa shirika hilo kote ulimwenguni wamepatiwa likizo ya lazima kuanzia usiku wa manane, jana Jumapili, Februari 23, 2025 isipokuwa wanaoshughulikia masuala muhimu.
Mchakato wa kuwafuta kazi wafanyakazi 1,600 wa shirika hilo walioko nchini Marekani utaendeshwa sambamba na likizo hiyo.
“Watakaoathirika watapokea jumbe kufikia Februari 23, 2025, pamoja na maelekezo na habari kuhusu mafao na haki zao.” iliendelea kusema ilani hiyo.
Wafanyakazi ambao shughuli zao haziwezi kusimamishwa ambao wanatarajiwa kuendelea kufanya kazi pia watafahamishwa kufikia saa 11 jioni, Februari 23, 2025.
Ilani ya awali ilikuwa imedokeza kwamba wafanyakazi wa shirika hilo wapatao elfu 2 walioko Marekani wangepoteza nafasi zao za ajira na hakuna sababu iliyotolewa.
Hatua hii inajiri baada ya Jaji mmoja nchini Marekani kutoa uamuzi Ijumaa ulioruhusu utawala wa Trump kuendeleza mipango ya kuondoa wafanyakazi wengi wa USAID katika muda wa siku 30.
Wafanyakazi walio ughaibuni wa shirika hilo watanufaika na mpango uliofadhiliwa na shirika hilo wa usafiri hadi nyumbani na mafao mengine.
Shirika hilo linahakikishia wafanyakazi wake kwamba limejitolea kuhakikisha usalama wa walio ughaibuni na kwamba wataendelea kupata mifumo ya shirika hilo hadi watakaporejea nyumbani.
Idara ya ufanisi serikalini (DOGE) inayoongozwa na mjasiriamali Elon Musk ndiyo inaendesha mpango huu wa kusambaratisha shirika kuu la kusambaza misaada ya Marekani.
Musk, ambaye alirejelea USAID kuwa shirika la uhalifu, na marafiki wengine wa Trump wanasema kwamba shirika hilo limejaa ubadhirifu na ulaghai na huwa linatekeleza ajenda ya uliberali ambayo sio sehemu ya kazi yake.