Vita vya ghuba vimesababisha hali tete nchini Tanzania huku bei ya mafuta ikipanda kwa shilingi 50 za Kenya sawia na shilingi 1,000 za Tanzania kwa kila lita.
Kwa mujibu wa bei mpya ya mwezi Aprili iliyotangazwa jana Jumatano na Mamlaka ya Nishati na Matumizi ya Maji (EWURA), bei hiyo inatokana na ongezeko la bidhaa za mafuta kote ulimwenguni. Hali hiyo inasababishwa na mashambulizi ya pamoja yanayotekelezwa na Israel na Marekani nchini Iran huku Iran pia ikijibu kwa kushambulia balozi za Marekani katika mataifa mengi jirani yakiwemo Qatar na Saudi Arabia.
EWURA ilitangaza kuwa bei ya Petroli itauzwa kwa shilingi 3,820 (Ksh 191.62) mwezi huu kutoka bei ya mwezi Machi ya shilingi 2,864 (Ksh 143.66), liikiwa ongezeko la asilimia 33.4 kwa lita moja.
Bei mpya ya dizeli itakuwa shilingi 3,806 (Ksh 190.92) kutoka bei ya awali ya shilingi 2858 (Ksh 143.36) kwa kila lita.
Mafuta taa yanauzwa kwa shilingi 3,684 (Ksh 184.80) kutoka kiwango cha mwezi Machi cha shilingi 2,932 (147.06) kwa lita moja.
Hata hivyo, bei ya mafuta imepanda zaidi katika maeneo ya mashinani huku mji wa Bukoba ukishuhudia bei ya juu zaidi ya petroli iliyopanda hadi shilingi 204.16 za Kenya kwa kila lita.
Ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushuhudia ongezeko kubwa la bei ya mafuta tangu mwaka 2022, wakati vita vya Urusi na Ukraine vilipoanza.