Upinzani utagawanyika mara nne kufikia mwezi Aprili mwakani, atabiri Waiguru

Martin Mwanje
2 Min Read
Anne Waiguru - Gavana wa Kirinyaga

Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru sasa anatabiri kuwa upinzani utagawanyika mara nne kufikia mwezi Aprili mwakani. 

Kauli zake zinawadia wakati ambapo viongozi wa upinzani wameahidi kudumisha umoja na kumchagua mmoja wao kupeperusha bendera ya upinzani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

“Kufikia mwezi Aprili mwaka ujao, upande wa upinzani utagawanyika mara nne. Si Raila aliingia kwa serikali? Sasa kwa nini hamuniamini nikiwaambia kura zitabebwa tu hivi mtakuta watu pale, kwa hivyo siasa msiweke kwa roho,” alisema Waiguru wakati akiwahutubia wakazi wa wadi ya Ngariama katika kaunti yake ya Kirinyaga.

“Sisi ndio tunajua kile kinaendelea. Ulisikia vizuri sana akisema Predident akikuja usimpigie makelele, si ndio? Lakini mwenye ameleta President mfanye nini… si mlisikia akisema? Jiulize kwa nini anasema hivyo,” aliongeza Waiguru akirejelea kauli za Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.

Waiguru amekuwa mkosoaji mkubwa wa Gachagua katika eneo la Mlima Kenya na amewataka wakazi wa eneo hilo kuunga mkono Rais William Ruto kuchaguliwa tena kuhudumu kwa muhula wa pili.

Upinzani una viongozi kadhaa wanaomezea mate urais ikiwa ni pamoja na Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Martha Karua wa PLP na Dkt. Fred Matiang’i wa chama cha Jubilee.

Haijulikani ikiwa viongozi hao watafikia makubaliano ya ni nani atagombea urais kati yao wakati uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukizidi kunukia.

 

Share This Article