Wadau wa Kiswahili leo Ijumaa, Julai 7, 2023 wameungana mikono kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wakati wa kikao chake cha 41 kilichoandaliwa mjini Paris, Ufaransa mnamo mwaka wa 2021, liliitenga Julai 7 kila mwaka kuwa siku ya kuadhimishwa lugha hiyo kote duniani.
Hatua hiyo ilikifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Shabaha ya maadhimisho hayo ni kuakisi umuhimu wa Kiswahili na hatua ambazo lugha hiyo imepiga katika sekta mbalimbali na nafasi yake katika jamii kwa sasa.
Aidha, Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi kote duniani kikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200.
Kenya leo Ijumaa inajiunga na ulimwengu kuadhimisha siku hiyo katika maadhimisho yatakayoandaliwa katika kaunti ya Mombasa.
Huku akifahamu umuhimu wa Kiswahili, Waziri wa Utalii Peninah Malonza katika mahojiano na KBC Radio Taifa leo Ijumaa kupitia kipindi cha Zinga, ametoa wito kwa wadau katika sekta ya utalii kutumia lugha hiyo adimu na adhimu kunadi kazi zao.
Malonza alisema kuna haja ya kutafuta njia za kutumia idadi inayoongezeka ya watu walio na shauku ya kujifunza Kiswahili kupigia debe sekta hiyo.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay, Kiswahili ni moja ya lugha zinazozungumzwa mno barani Afrika.
Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani, Azoulay alisema kuienzi lugha hiyo ni kuheshimu maadili ya lugha nyingi.
“Kiswahili ni zaidi ya njia ya mawasiliano, ni dirisha la tamaduni mbalimbali, mawazo, aina ya uelewa wa elimu,” alisema Azoulay.
“Lahaja zake nyingi zinazotoa lenzi ya kipekee ya kuutazama ulimwengu.”
Huku akipongeza wajibu ambao Kiswahili kinatekeleza barani Afrika, Azoulay aliipongeza lugha hiyo rasmi ya Umoja wa Afrika, AU, akiitaja kuwa lugha ya Kidiplomasia inayosaidia kuendeleza ajenda ya bara hili.