Sifuna aondolewa wadhifa wa naibu kiranja wa wachache

Seneta wa Migori Eddy Oketch ndiye anachukua wadhifa huo.

Marion Bosire
1 Min Read

Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna ameondolewa kwenye wadhifa wa naibu kiranja wa wachache katika bunge la Seneti.

Haya yalitangazwa na Spika Amason Kingi katika kikao cha leo cha bunge hilo huku akitangaza kwamba Seneta wa Migori Eddy Oketch ndiye anachukua wadhifa huo.

Kingi alisema kwamba aliarifiwa kuhusu mabadiliko hayo kwa njia ya barua iliyoandikwa leo Julai 16, 2026, kutoka kwa kiongozi wa wachache katika bunge la Seneti Stewart Madzayo.

Barua hiyo hiyo ndiyo ilitoa taarifa kuhusu kuteuliwa kwa Seneta Eddy Gicheru Oketch kuchukua mahala pa Sifuna.

Akijibu tangazo hilo, Sifuna aliwashukuru viongozi wa wachache katika bunge la Seneti na maseneta wote kwa kushirikiana naye katika kipindi chake uongozini.

“Ninawashukuru viongozi na Maseneta kwa ushirikiano walionipa katika kipindi changu uongozini kama Naibu Kiranja wa Wachache katika Seneti. Ninampongeza mdogo wangu, Seneta Eddy Oketch, kwa jukumu lake jipya,” alisema Sifuna.

Mabadiliko hayo kutoka kwa muungano wa Azimio yanaanza kutekelezwa mara moja.

Maendeleo haya ya hivi karibuni yanajiri wiki moja baada ya Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, ORPP kutambua rasmi kuondolewa kwa Sifuna kama Katibu Mkuu wa ODM.

Share This Article