Serikali yaanzisha mchakato wa kuwaondoa Wakenya kwenye sajili ya UNHCR

Martin Mwanje & Kinyungu Kithendu
3 Min Read

Serikali imezindua awamu nyingineya kuwaondoa Wakenya kwenye sajili ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wakimbizi, UNHCR baada ya kuhangaika kwa miaka mingi katika hatua ambayo iliwafanya kuishi maisha bila kujua hatima yao. 

Wakenya wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 40,000 wengi wao vijana waliojipata kwenye sajili ya UNHCR hawangeweza kupata uraia na hivyo kujipata kwenye njia panda kisheria.

Wiki jana, Wizara ya Mambo ya Ndani ilitoa waraka kwa Kamati ya Usalama na Ujasusi ya kaunti ndogo huko Garissa ikiikubalia kuwakagua na kupendekeza kusajiliwa kwa Wakenya ambao awali walisajiliwa kama wakimbizi.

Waraka huo pia ulitoa miongozo ya kufuatwa na maafisa wakati wa ukaguzi.

Watu walioathiriwa wanatakiwa kutambulishwa na chifu wa eneo hilo kwa maandishi na picha ya mtu maombi. Aidha wanatakiwa kufika wenyewe mbele ya kamati hiyo wakiandamana na wazazi wao.

“Katika hali ambayo wazazi wa mtu aliyeathiriwa au jamaa wamefariki, chifu atathibitisha kwa maandishi mlezi wa ukoo wa mtu huyo ili kuunga mkono utambulisho wake na atatakiwa kutoa maelezo kupitia fomu za maombi,” ilisema sehemu ya waraka huo.

Kulingana na waraka huo, watu walioathirika wanatakiwa kutoa ushahidi unaokubalika wa nyaraka kama vile uthibitisho wa umri wao na pia kutangaza nambari ya hadhi yao ya ukimbizi waliopewa kwenye kambi ya wakimbizi.

Shirika lisilokuwa la serikali kwa jina Haki na Sheria ambalo limekuwa likitetea haki za watu waliosajiliwa mara mbili katika Ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti ya Garissa Mjini na Idara ya Kitaifa ya Usajili  lilikutana na machifu na manaibu wao katika mji wa Garissa Mjini kujadili mipango ya kuanzisha shughuli hiyo.

Akiwahutubia wanahabari katika kituo cha Jamhuri mjini Garissa, the Naibu Kamishna wa Kaunti Solomon Chesut aliwaonya mawakala wanaoweza wakawalaghai watu walioathiriwa na ambao hawana ufahamu barabara juu ya mchakato wa ukaguzi akisema hatua kali itachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayepatikana akiitisha hongo akisema mchakato huo unafanywa bila malipo.

Alisema bado wanasubiri maelekezo ya ni lini hasa mchakato huo utaanza akiongeza kuwa unaweza ukaanza katika kipindi cha wiki moja au mbili zijazo na muda wa uendeshaji wake pia kutolewa.

Serikali ilitoa vitambulisho vya kitaifa kwa watu zaidi ya 12,000 Januari, 2022 huku ukaguzi ulioangaziwa zaidi ukifanyika mwishoni mwa mwaka 2019. Ukaguzi uliofanyika mwaka 2016 haukufua dafu.

 

Martin Mwanje & Kinyungu Kithendu
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *