Serikali kusaidia waathiriwa wa ajali ya Nyeri

Ajali hiyo ilihusisha Lori na gari la abiria almaarufu Matatu kwenye barabara kuu ya kutoka Nyeri kuelekea Nyahururu na kusababisha vifo vya watu 15

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na ile ya kaunti ya Nyeri, itatoa usaidizi kwa waathiriwa wa ajali mbaya ya barabarani iliyotokea jana jioni karibu na Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi.

Rais William Ruto alitoa ahadi hiyo kwenye ujumbe wake wa pole akisema, “Tunatoa pole zetu kwa waathiriwa wa ajali ya barabarani iliyotokea karibu na chuo kikuu cha Dedan Kimatji katika kaunti ya Nyeri.”

Kiongozi wa nchi aliongeza kusema kwamba anawaombea afueni ya haraka walioachwa na majeraha kutokana na ajali hiyo na kwamba tayari serikali inawasiliana na familia za waathiriwa ili kuwapa usaidizi stahiki.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula alikumbusha wote wanaotumia barabara kusalia waangalifu na kuzingatia sheria za barabarani ili kuzuia vifo zaidi.

“Nimeipa changamoto Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA kuimarisha sheria za barabarani, kuchunguza operesheni za barabarani na kuchunguza hali ya magari na utaalamu wa madereva,” alisema Wetang’ula.

Spika huyo vile vile alitoa pole zake kwa familia zilizoathirika,”Rambirambi zangu za dhati zifikie familia, marafiki na wananchi wa Kaunti ya Nyeri kufuatia tukio hili la kusikitisha.”

Alilalama kwamba kwa mara nyingine, ajali imechukua maisha ya raia na kufanya ndoto nyingi kutotimia.

Ajali hiyo ilihusisha lori na matatu kwenye barabara kuu ya kutoka Nyeri kuelekea Nyahururu na kusababisha vifo vya watu 15.

Share This Article