Maafisa wa usalama kutoka asasi mbalimbali, wamepata mavazi yanayoaminika kuwa ya wanamgambo wa Alshabab katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi.
Operesheni hiyo ya kijasusi ilitekelezwa na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Maafisa wa Polisi wa kukabiliana na Ugaidi (ATPU).
Maafisa hao walifanya operesheni hiyo baada ya kukamatwa kwa mavazi mengine yanayoaminika kuwa ya Alshbabab jijini Dhobley Aprili 6, 2026, na maafisa wa usalama wa Jubaland.
Upatikanaji huo ishara ya kuwepo kwa usambazaji wa sare hizo mipakani, huku maafisa wa uchunguzi wakifuatilia nguo hizo hadi katika kampuni ya usafirishaji mizigo ya Gaani, mtaa wa Eastleigh.
Vifaa zaidi pia vilipatikana katika duka jirani Vision Point Express, linalotumiwa kuhifadhi mizigo kwa muda.
Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa Meneja wa Gaani Parcel Express Omar Elmi Issack, alihifadhi sare hizo baada ya kuzipokea kutoka kwa mtu aliyetambuliwa kama Sharif.
Maafisa hao pia walianzisha uchunguzi kwa duka la Safe Link Cargo kwenye jumba la Soma Towers, linaloaminika kuingiza hapa nchini makasha 37 kutoka china kupitia bandari ya Mombasa.