Safari yangu kuelekea nchini Urusi ilifunikwa na wingu la matarajio si haba. Yale ya kujionea mambo mengi ya kushangaza na pengine ya kustaajabisha.
Huku halijoto ya matarajio hayo ikizidi kunipanda kila baada ya sekunde, mashaka makuu yalimtafuna mama yangu mzimamzima. Alihofia usalama wangu na kuakisi hofu walio nayo watu wengi juu ya Urusi.
Hivyo, nilianza safari hiyo kwa mseto wa msisimko na kutokuwa na uhakika, nikijiweka kimakusudi kizani kuhusu nini nilichotarajia.
Niliwasili Uwanja wa Ndege wa Domodedovo mjini Moscow saa 9:00 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki. Mazingira angavu, yaliyowiana na saa 1:00 asubuhi nchini mwangu, yalidhihirisha mji wa Moscow ulivyovutia katika msimu wake wa joto.
Kuwasili mjini humo mapema nako kulinipa fahari ya kushuhudia kuchomoza kwa jua kwa namna ya kuvutia saa moja baadaye. Hakika hilo lilikuwa tukio lililouchora mji wa Moscow kwa mwanga mtulivu.
Kundi letu lilijumuisha wanahabari vijana 32 ambao ni wataalamu kutoka nchi 28 za Amerika Kusini, Mashariki ya Kati, Ulaya, Afrika, na Asia.
Kilichotuleta pamoja katika mji mkuu wa kusisimua wa Urusi wa Moscow, kikiwa Programu ya SputnikPro_MIR New Generation. Licha ya kutolala, jua lilinisalimia kwa ukarimu saa 10:00 alfajiri nilipotoka katika chumba nilimolala hotelini siku iliyofuata.
Kutoka kwenye ubaraza wangu kwenye orofa ya 25, nilitazama haiba ya mji huo na nilivutiwa hasa na maegesho yaliyojaa skuta za umeme na baiskeli. Awali, hili lilinisisimua, lakini baadaye nilitambua kwamba skuta hizo ni njia ya kawaida ya usafiri mjini Moscow.
Wakati wa ziara yetu mjini humo, nilishangaa kuona jinsi wakazi walivyosogea kwa amani, wakiwa na simu zao za mkononi na tableti na kuendesha skuta na baiskeli zao kwa urahisi. Mandhari haya matulivu yalikinzana na wasiwasi wa usalama niliokuwa nao, uliochochewa na mitandao ya kijamii iliyoashiria Urusi kama nchi yenye ukosefu wa usalama.
Mpangilio na ufanisi wa mji wa Moscow ulivutia, hasa njia za watembea kwa miguu na kuzingatia kwa makini zaidi vivuko vya watembea kwa miguu, ambavyo nchini mwangu tunaviita vivukomilia, jina lililotokana na wanyama wenye mistari myeusi na myeupe ambao ni kivutio kikubwa cha watalii katika mbuga zetu za wanyama.
Wakati mmoja, nilimtajia Nicola Daniels, mshiriki kutoka Afrika Kusini, kwamba mjini Moscow, huwezi ukavuka barabara mahali popote bali tu kwenye vivukomilia.
Mwitiko wake wa kushtuka akiuliza, “Punda milia?” ulinifanya nitambue kwamba nilikuwa nimemtambulisha kwa istilahi ya Kenya kwa kutodhamiria.
Utangamano huu ulionyesha mabadilishano ya kitamaduni yaliyokuwa yakifanyika kati yetu washiriki. Mji wa Moscow uliweka bayana mfumo wa usafiri wenye mpangilio mzuri, ambapo aina tofauti za usafiri zilibadilishana zamu bila matatizo.
Sheria za barabarani zilifuatwa kwa makini; taa zilipogeuka njano, magari yalisimama umbali kiasi kutoka kwa kivukomilia, tofauti na nchini mwangu, ambako magari mara nyingi hukaribiana na kutoacha nafasi ya hata nzi kupita.
Cha kushangaza, huko Moscow, hakuna mtu aliye juu ya sheria. Maafisa wa polisi hufuata taa za barabarani na husimama wakiwa kwenye pikipiki na magari yao ya doria ili kuruhusu watembea kwa miguu kuvuka katika maeneo yaliyotengwa.
Hii inaonyesha kiwango cha kutii na kuhesimu sheria ambacho nilibaini kinapaswa kupongezwa, na ni dhahiri kwamba polisi mjini Moscow wanaheshimiwa sana na wana mamlaka makubwa.
Skuta za umeme zilipamba mandhari ya mji, hata kwenye mbuga. Wasiwasi wangu wa awali kuhusu usalama ulifanya nishangae jinsi skuta hizi zilivyosalia bila kuguswa, zikiwa tayari kuwasaidia watu zaidi kuendelea na shughuli zao siku iliyofuata. Nilipoendelea kutalii Moscow, dhana zangu za awali za ukosefu wa usalama zilianza kutoweka.
Mazingira ya mji huo yalikuwa yale ya usalama na utulivu, ishara tosha ya miundombinu yake imara na sheria zinazotekelezwa vizuri.
Kuona watu wakitembea kwa amani, wakitumia vifaa vyao, na upatikanaji wa njia mbalimbali za usafiri zinazotumiwa kwa pamoja kama vile skuta za umeme kulichangia hali ya kawaida na usalama ambayo sikuwa nimetarajia.
Tukio moja la kukumbukwa lilikuwa kutembelea eneo la Red Square, nembo maarufu katika historia yenye utajiri mkubwa ya Urusi. Eneo hilo lilijaa watalii na raia wa nchi hiyo, wote wakifurahia uzuri wa majengo yaliyozunguka eneo hilo na msimu wa joto. Mazingira yalikuwa ya kusisimua lakini yenye mpangilio, na kufutilia mbali zaidi mashaka kuhusu usalama wa mji huo.
Mbali na nembo zake za kihistoria, hali ya kisasa ya mji wa Moscow ilipendeza. Mji huo, kwa mfano, una vituo vilivyopambwa na picha na sanamu za kuvutia.
Msisimko wa ziara yetu, hasa tukiandamana na Stephany Ishac kutoka Lebanon aliyekuwa mcheshi na mwenye kelele nyingi, ulitufanya tupotee njia ya kurudi.
Wakati mmoja, milango ya mji iliyojifungua na kujifunga yenyewe ilijifunga baada ya Ahmed Rajabi kutoka Palestina kuingia, na kutuacha sisi wengine nyuma. Ahmed Gaddeh kutoka Tunisia alishangazwa na ufanisi na usafi wa mfumo wa mji huo, akielezea kwamba hata sehemu za taka, zilipojaa, usafi wake ulidumishwa katika eneo moja lililotengwa.
Hofu zangu za awali hazikuwa na msingi. Moscow ni mji unaostawi kutokana na utaratibu, heshima, na jamii. Dhana potovu kuhusu usalama wake kwa kiasi kikubwa hazina msingi, kama tajiriba yangu ilivyoonyesha.
Mfumo wa usafiri wa ufanisi wa mji, wananchi wanaotii sheria, na mandhari ya utamaduni yanayosisimua huchangia usalama na ustawi.
Ziara yangu mjini Moscow ilikuwa ya kugundua na kuelimika. Ilinifunza kwamba ingawa wasiwasi wa usalama una msingi, haupaswi kufunika uhalisia wa mahali.
Kwa uzuri wake, ufanisi, na ukarimu, Moscow ilienda kinyume cha dhana potovu na kutoa tajiriba ya aina yake ambayo daima itasalia nami.