Safari Rally yaanza kwa kishindo madereva wakitatizwa na mvua

Mashindano hayo ya siku nne yatakamilika Jumapili hii na ni ya tatu kwenye msururu wa mashindano 14 ya mwaka huu ya WRC.

Dismas Otuke
1 Min Read

Makala ya mwaka huu ya mashindano ya mbio za magari ya WRC Safari Rally yalianza jana Alhamisi jioni kwa kishindo na changamoto tele, madereva wakikabiliana na mvua na matope.

Katika kituo cha Kwanza cha Camp Moran, barabara ilikuwa telezi huku dereva wa Uswidi Oliver Solberg akiendesha gari la Toyota Gazoo akitwaa uongozi.


Kwenye kituo cha pili cha Mzabibu, hali ilikuwa kinyume barabara ikiwa kavu na kuwapa madereva fursa ya kujinusuru baada ya kupoteza muda mwingi katika kituo cha Camp Moran.

Toyota Gazoo walidhihirisha ukakamavu wao wakinyakua nafasi tano za kwanza jana, Solberg akiongoza.


Kwa jumla, madereva walishindana umbali wa kilomita 33 katika siku ya kwanza.

Mashindano hayo yameingia siku ya pili mapema leo Ijumaa huku madereva wakitarajiwa kushindana umbali wa kilomita 100, kupita vituo vinane vya Camp Moran, Loldia, Kengen Geothermal, Kedong kurudia tena Loldia, Kengen Geothermal na Kedong na kufungia siku Mzabibu.

Mashindano ya mbio za magari WRC Safari Rally Kenya yalizinduliwa na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki.

Mashindano hayo ya siku nne yatakamilika Jumapili hii na ni ya tatu kwenye msururu wa mashindano 14 ya mwaka huu ya WRC.

Share This Article