Ruto kutoa hatimiliki za ardhi wakati wa ziara Pwani

Rais atatoa hatimiliki hizo kwa wakazi wapatao 200,000 wa kaunti za Taita-Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu. 

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais Ruto akitoa hatimiliki za ardhi kwa wakazi wa eneo la Pwani awali

Rais William Ruto atatoa takriban hatimiliki 200,000 za ardhi katika eneo la Pwani wakati atakapozuru eneo hilo kuanzia kesho Jumamosi. 

Aidha, Ruto anatarajiwa kuzindua kiwanda kipya cha kusafisha mafuta katika kaunti ya Lamu Jumatano wiki ijayo.

Atafanya ziara katika kaunti za Taita-Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu.

Kwenye taarifa, Ikulu ya Nairobi inasema ziara hiyo itampa kiongozi wa nchi fursa ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika eneo hilo huku akijadiliana na viongozi na wakazi wa eneo hilo miradi inayopaswa kupewa kipaumbele.

Utoaji wa hatimiliki za ardhi kwa wakazi ni sehemu ya mpango wa serikali wa kutoa hatimiliki 500,000 kwa wamiliki wa ardhi wakati ikitafuta kutatua suala la maskwot na changamoto zingine zinazohusiana na ardhi ambazo zimewaathiri wakazi wa eneo la Pwani kwa muda mrefu.

Ziara ya Rais Ruto itaanzia kaunti ya Taita-Taveta kesho Jumamosi ambako anatarajiwa kutoa hatimiliki za ardhi 31,318 kwa wakazi wa maeneo bunge ya Mwatate na Voi.

Kisha siku ya Jumatatu, ataelekea kaunti ya Kwale ambapo hatimiliki za ardhi 94,175 zitatolewa kwa wakazi wa Lunga Lunga, Msambweni na Kinango.

Katika kaunti ya Kilifi, Ruto amepangiwa kutoa hatimiliki za ardhi 36,826 kwa wakazi wa maeneo bunge ya Kaloleni, Rabai, Ganze, Kilifi Kusini na Malindi.

Wakazi wa kaunti za Mombasa, Lamu na Tana River pia watanufaika.

Jumatano wiki ijayo, Rais Ruto ataweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha East Africa Refinery kitakachojengwa kwa kima cha shilingi trilioni 2 huko Lamu.

Mradi huo utatekelezwa kwa pamoja na serikali ya Kenya na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuchakata mafuta ghafi kutoka Lokichar, kaunti ya Turkana na kusambaza bidhaa zilizosafishwa za petroli kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.

Kulingana na Ikulu ya Nairobi, kiwanda hicho kitaboresha usalama wa nishati wa nchi hii kwa kuhakikisha usambazaji thabiti wa bidhaa za petroli huku kikibuni nafasi 50,000 za ajira.

 

Share This Article