Rais William Ruto alikuwa na pirikapirika nyingi za kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo la Magharibi anakofanya ziara ya kikazi ya siku tano.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto atazuru kaunti zote za eneo hilo.
Leo Jumatatu, kiongozi wa nchi alitembelea kijiji cha Nderema, eneo bunge la Navakholo, kaunti ya Kakamega, alikozindua mradi wa Last Mile Connectivity. Mradi huo unakusudia kusambaza umeme kwa kaya 161 kwa gharama ya shilingi milioni 12.7.

Kwa jumla, serikali inawekeza shilingi bilioni 2.37 kuunganisha umeme kwa kaya zaidi ya 36,700 katika kaunti hiyo.
Rais Ruto anasema hatua hiyo itaziwezesha familia na kufungua milango ya fursa mpya kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, Rais aliweka jiwe la msingi kwa soko la kisasa la Malaha litakalogharimu shilingi milioni 270.
Soko hilo ni moja ya miradi 24 inayotekelezwa na serikali kuu kwa gharama ya shilingi bilioni 4.4 katika kaunti ya Kakamega.
Mradi mwingine ulionzinduliwa ni ule wa maji wa Shitoli katika eneo bunge la Ikolomani.
Akiwahutubia wakazi wa eneo hilo, Ruto aliwapuuzilia mbali wapinzani wake akiwataja kuwa watu wasiokuwa na ajenda.
“Wakenya si wajinga. Wanaweza kuona kaulimbiu zisizokuwa na chochote za wapinzani wetu,” Ruto aliwakosoa wapinzani wake.
“Wakati ukiwadia, watatoa uamuzi wao juu ya ni nani hasa ana mpango bora kwa nchi.”
Jana Jumapili, Ruto alikagua ukarabati unaoendelea wa uwanja wa ndege wa Kakamega unaotarajiwa siyo tu kuboresha shughuli za uchukuzi bali pia uchumi wa eneo hilo.