Ripoti kuhusu utekelezaji wa NADCO tayari

Kamati hiyo inasema iko tayari kabisa kuwasilisha ripoti kuhusu mambo ambayo iligundua na mapendekezo yake.

Marion Bosire
1 Min Read

Kamati iliyoteuiwa kuongoza utekelezaji wa ripoti ya pointi kumi ya kamati ya mdahalo wa kitaifa almaarufu NADCO, imekamilisha ripoti yake.

Chini ya uongozi wa aliyekuwa Seneta Mteule Agnes Zani, kamati hiyo inasema iko tayari kabisa kuwasilisha ripoti kuhusu mambo ambayo iligundua na mapendekezo yake.

Kamati hiyo imekuwa ikihusisha wadau muhimu tangu Januari na inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais William Ruto wakati wa mkutano wa pamoja wa wabunge wa Kenya Kwanza na ODM kesho Jumanne.

Kundi hilo linasema limekuwa likiongozwa na jukumu walilopatiwa.

Walihitajika kushauriana na wadau mbali mbali kama wizara za serikali, idara na mashirika, mashirika ya kijamii na wakenya kwa jumla kabla ya kuandaa ripoti.

Zani alisema mipango ya kuandaa mkutano wa pamoja wa wabunge kabla ya Machi 7, ilitikiswa kidogo na kifo cha mbunge wa Emurua Dikirr Johanna Ng’eno.

Kamati ya mdahalo wa kitaifa NADCO ilikuwa chini ya uenyekiti wa Kalonzo Musyoka aliyewakilisha muungano wa upinzani Azimio na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichungwah.

Lengo la mdahalo huo wa mwaka 2023 lilikuwa kutuliza joto la kisiasa lililokuwa likishuhudiwa wakati huo na kupendekeza mabadiliko ya kustawisha utawala na mifumo ya uchaguzi.

Share This Article