Rais Ruto kuwapa Harambee Stars zawadi aliyoahidi

Katika mechi ya jana alikuwa ameahidi kila mchezaji shilingi milioni 2.5 iwapo wangeishinda Zambia.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amepongeza timu ya taifa ya soka Harambee Stars kwa ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Zambia katika mechi yake ya mwisho ya makundi kwenye mashindano ya CHAN jana Jumapili.

Kupitia mitandao ya kijamii, kiongozi wa nchi alielezea jinsi timu ya taifa ilikuwa imepuuzwa na wengi ikitizamiwa kwamba ilikuwa kwenye kundi la timu kali barani Afrika.

“Mwanzo wa kinyang’anyiro hiki cha CHAN, hakuna aliyeaminia Harambee Stars kukiuka kiwango cha makundi. Hata hivyo tulikuwa kwenye kundi la mauti lakini wachezaji wetu wameshinda.” aliandika Rais Ruto.

Kenya sasa inaingia katika kiwango cha nusu fainali cha mashindano hayo baada ya kushinda timu kali barani Afrika na Rais anaimotisha timu hiyo kuendeleza matokeo bora.

“Pongezi Harambee Stars! Mmeipa fahari nchi yetu, mmechochea furaha na kuunganisha taifa katika kusherehekea ushindi. Sasa songeni mbele na mshinde bara zima.” alisema Rais kwa chapisho lake.

Rais alimalizia kwa kuhakikishia Harambee stars kwamba atatimiza ahadi aliyotoa kwao iwapo wangeshinda mechi ya jana. “Kwa upande wangu nitacheza kama mimi. Mwisho wa yote, dawa ya deni ni kulipa” aliandika.

Kabla ya kuanza kwa mashindano ya CHAN yanayoandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania, Rais Ruto alitoa ahadi za zawadi za pesa kwa wachezaji kwa kila mechi ambayo wangeshinda na katika kila kiwango ambacho wangeingia.

Katika mechi ya jana alikuwa ameahidi kila mchezaji shilingi milioni 2.5 iwapo wangeishinda Zambia.

Share This Article