Rais William Ruto amempongeza Prof. Phoebe Okowa baada ya kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki, ICJ.
Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wa X, kiongozi wa taifa alisema uchaguzi huo ni fahari kubwa ya Kenya na dhihirisho la mchango wa kisheria na kimaadili unaotolewa na taifa hili kwa jumuiya ya kimataifa.
“Unapochukua wadhifa huo, tunakutakia ufanisi unapotekeleza majukumu yako kwa uadilifu na kuiwezesha mahakama ya ICJ kuendelea kuzingatia sheria ya kimataifa na kufanikisha upatikanaji wa suluhu kati ya mataifa,” alisema Rais Ruto.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alisema kuchaguliwa kwa Prof. Okowa kwenye mahakama hiyo ni ishara kwamba Kenya inaunga mkono uzingatiaji wa haki ya kimataifa, mfumo wa sheria na mfumo wa usawa duniani.
“Ufanisi huo ni ishara tosha kwamba jumuiya ya kimataifa ina imani ya utaalam wa kisheria wa Kenya, uongozi wa kidiplomasia na uwezo wa kutoa mchango katika upatikanaji wa amani miongoni mwa mataifa,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
Prof. Okowa aliibuka mshindi baada ya kupata kura 183 kutoka kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kura 13 kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kuwapiku washindani wake kutoka mataifa mengine, akiwemo mwaniaji kutoka Sierra Leone, Charles Chernor Jalloh.
Okowa atahudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka tisa.