Rais William Ruto leo Jumatano ametia saini kuwa sheria mswada wa makadirio ya ziada ya bajeti ya mwaka 2025-2026, huku wabunge wakiongeza bajeti hiyo kwa shilingi bilioni 393.2
Bajeti hiyo ya mwaka 2025-2026 sasa imeongezeka hadi shilingi trilioni 4.695 kutoka shilingi triliono 4.301.
Kwenye makadirio hayo, sekta ya usalama wa taifa imevuna pakubwa baada ya kutengewa shilingi bilioni 60, ambapo idara ya Uslama wa Ndani na Utawala wa taifa zikitumia shilingi bilioni 11.9
Wahasiriwa wa maandamano ya mwaka 2024, wametengewa fidia ya shilingi bilioni mbili, huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, ikitengewa shilingi bilioni 2.9 kukamilisha madeni yake kwa lengo la kuhakikisha inajiandaa vyema kwa Uchaguzi Mkuu ujao.
Sekta ya elimu itapokea mgao wa shilingi bilioni 45.3, Tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC ikitengewa shilingi bilioni 24.2.
Bunge limeitengea Wizara ya Afya shilingi bilioni 5.5, bilioni nne zikiwa ni za kulipa madeni yanayodaiwa iliyokuwa Hazina ya Bima Kitaifa ya Afya (NHIF).
Mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, utapokea shilingi bilioni 25, kufanikisha Ajenda ya Maendeleo ya kiuchumi almaarufu (BETA).
Sekta ya kilimo imeongezewa shilingi bilioni 17, kuhakikisha uzalizashi toshelevu wa chakula hapa nchini, huku mpango wa mbolea ya bei nafuu ukipewa shilingi bilioni 10.