Rais William Ruto leo Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi ametia saini miswada mitatu kuwa sheria.
Sheria mpya zilizosainiwa na Rais ni Sheria ya Ada za Ziada, 2026, Sheria ya Kahawa, 2023 na Sheria ya Utabiri wa Hali ya Hewa, 2023.
Miswada hiyo iliwasilishwa na Bunge la Taifa na la Seneti.
Sheria ya Kahawa, 2023 inaruhusu ustawishaji na udhibiti wa sekta ya kahawa nchini.
Hususan, inapanga upya sekta ya kahawa kwa kuhamisha majukumu ya udhibiti na biashara kutoka kwa Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) hadi kwa Bodi ya Kahawa nchini Kenya.
Katika sheria hiyo mpya, Bodi ya Kahawa pia imekabidhiwa jukumu la kushughulikia maombi ya leseni, usajili wa wafanyabiashara wa kahawa na kusimamia utekelezaji wa mikakati, sera na mifumo ya ufadhili katika sekta hiyo, miongoni mwa mambo mengine.
Kwa upande mwingine, Sheria ya Utabiri wa Hali ya Hewa, 2023, inaanzisha mpangokazi wa kudhibiti huduma za utabiri wa hali ya hewa nchini na kuratibu na kufuatilia utoaji wake.
Sheria hiyo pia inahakikisha Kenya inazingatia viwango vya kimataifa na sheria zinazosimamia huduma za utabiri wa hali ya hewa.
Kadhalika, sheria hiyo inaanzisha Mamlaka ya Huduma ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya ambayo itahudumu kama mshauri mkuu wa kiufundi kwa serikali kuu na za kaunti kuhusiana na masuala ya utabiri wa hali ya hewa.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Maspika Moses Wetang’ula wa Bunge la Taifa na Amason Kingi wa Seneti ni miongoni mwa viongozi waliokuwapo wakati wa utiaji saini wa miswada hiyo.