Raila Odinga asema maandamano ya Jumatano yataendelea

Tom Mathinji
2 Min Read
Raila Odinga akiwa ndani ya Matatu. Picha/Hisani.

Kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, siku ya Jumatatu asubuhi alitumia uchukuzi wa umma kutoka nyumbani kwake Karen hadi katikati ya Jiji la Nairobi.

Katika kile kilichowatamausha wakazi wa jiji la Nairobi, Odinga alishuka katika kituo cha magari cha Ambassador, na kutembea kwa miguu hadi katika sanamu ya  Tom Mboya.

Akiwa ndani ya matatu, Raila aliwalipia nauli abiria wote waliokuwemo, huku akilalamikia ghamara ya juu ya maisha, aliyoitaja kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM aidha alisisitiza kuwa maandamano ya siku ya Jumatano yangalipo.

Baada ya kula staftahi katika hoteli moja katikati ya Jiji, Raila aliwahutubia wananchi waliokuwa wakimsubiri nje, akisema kuwa kupanda kwa gharama ya maisha kumeathiri maisha ya Wa-Kenya wengi na ndio maana anashinikiza kusimamishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023.

“Nimewasili katikati ya Jiji kwa kutumia matatu na ninafahamu hali ambayo mnakumbana nayo. Gharana ya juu ya maisha imesababisha wahudumu wa matatu kuongeza nauli, na ninailaumu serikali iliyopo,” alisema Raila.

Raila alitoa wito mitambo ya sava ya tume ya uchaguzi nchini IEBC, kufunguliwa ili kuthibitisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.

Aidha Raila aliwahimiza wananchi kushiriki kukusanya sahihi milioni 10, shughuli inayolenga kumngátua mamlakani Rais William Ruto. Odinga alisema wananchi wana haki ya kuleta mabadiliko wanayoyahitaji.

Alisema siku ya Jumatano, wakenya watashirki maandamano, sio tu Jijini Nairobi lakini kote nchini.

“Sisi ni wananchi wenye amani na tunaheshimu sheria. Tutatekeleza haki yetu kwa njia ya amani siku ya Jumatano,” aliwaeleza wananchi.

Alikuwa ameandamana na mwenyekiti wa kamati kuu ya Azimio Wycliffe Opayanya, Mbunge wa Kisumu ya kati Dkt. Joshua Oron na mbunge wa Kibra Peter Orero. Wengine ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Nairobi Peter Imwatock na kiranja wa wengi katika bunge hilo Moses Ogeto.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *