Polisi wasambaratisha genge sugu la wahalifu Kampala

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wa ujambazi wakamatwa Uganda.

Maafisa wa polisi Jijini  Kampala, Uganda, wamesambaratisha genge moja la majambazi ambalo linadaiwa kuwahangaisha wakazi wa eneo la  Mukono na viunga vyake.

Operesheni hiyo ilitekelezwa baada ya kuripotiwa misururu ya wizi ambapo kundi la vijana almaarufu “Eggaali”, limedaiwa kuwashambulia wananchi kutumia silaha hatari kama vile visu na panga.

Kulingana na taarifa ya polisi nchini Uganda, genge hilo huwaibia wananchi simu za mkononi, mikoba, tarakilishi na saa hasaa katika barabara ya Kayunga, Kusatu, Nasuuti, na Wantoni.

“Baada ya kupokea malalamishi hayo, polisi walianzisha operesheni ya kijasusi ikilenga kundi hilo,” ilisema idara ya polisi kwenye ukurasa wa X.

Taarifa hiyo ya polisi ilisema kuwa, uchunguzi wa kina ulisababisha kukamatwa kwa mshukiwa wa kwanza Muhanguzi Vian, mwenye umri wa miaka 25 , na baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika kwenye shughuli za uhalifu katika eneo la Mukono na akawatambua washirika wenzake.

Wengine waliokamatwa ni pamoja na Mubiru David, almaarufu  “City”, mwenye umri wa miaka 20, Kizito Solomon, almaarufu “Kitama”,(18), Ssemanda Junior, amaarufu “Kamese”, (17), Muyomba Paul, almaarufu “Matama”, (17), na Okumu Mark, almaarufu “Sekere”,( 18).

Washukiwa hao wote walikiri kutekeleza uhalifu katika eneo la Mukono na viunga vyake.

TAGGED:
Share This Article