Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, ametoa wito wa kuharakishwa kwa ujenzi wa uwanja wa Wajir kabla ya sherehe za Madaraka Juni 1,2026.
Akizungumza alipoongoza kamati tekelezi kuhusu sherehe za kitaifa kukagua ujenzi wa uwanja huo, katibu huyo alidokeza kuwa hadi kufikia sasa, ujenzi wa uwanja huo umekamilika asilimia 28.
“Tumeridhishwa na hatua zilizopigwa hadi sasa, lakini ni sharti tuongeze kasi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya muda uliowekwa,” alisema Omollo.
Dkt. Omollo alisisitiza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha ufanisi wa sherehe hizo, akidokeza kuwa asasi zote husika zinajizatiti kutimiza majukumu yao.
“Tumeleta pamoja asasi zote kufanikisha sherehe hizi. Hatua zote za maandalizi haya zinafuatiliwa kwa karibu kuhakikisha ubora wa hali ya juu, usalama na kutimizwa kwa wakati,’ aliongeza katibu huyo.
Aidha, alisema hatua ya serikali ya kupeleka sherehe za kitaifa katika maeneo tofauti ya nchi, inazidi kuleta ushirikishi, mshikamano wa kitaifa na kuacha maendeleo ya kudumu katika kaunti andalizi.
“Kile tunachoshuhudia hapa Wajir ni ishara ya kujitolea kwa serikali,” alidokeza Dkt. Omollo.
Wengine waliokuwepo ni pamoja na Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi, Mrakibu wa eneo la Kaskazini Mashariki John Otieno na msemaji wa serikali miongoni mwa wengine.