Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Jumanne, amejiunga na jamaa na marafiki pamoja na viongozi mbalimbali katika ibada ya kufariji familia za waathiriwa wa ajali iliyotokea katika eneo la Londiani juma lililopita.
Takriban watu 54 walifariki huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali hiyo, iliyotokea siku ya ijumaa. Ibada hiyo ya maombi iliyoongozwa na viongozi wa makanisa mbalimbali, iliandaliwa mjini Londiani.
Awali, Gachagua alituma risala za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kwa wakenya kwa jumla kupitia ujumbe wa twitter.
Siku ya Jumatatu, serikali ilisema kuwa itawasaidia waathiriwa na familia zilizowapoteza wapendwa wao, katika ajali hiyo ya Londiani.
Gavana wa kaunti ya Kericho Dkt. Eric Mutai, alitoa hakikisho kuwa serikali ya kaunti hiyo italipa gharama za hospitali na zile za makafani kwa waathiriwa wa ajali hiyo.