Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu amesisitiza dhamira ya Idara ya Mahakama kuangamiza ajira ya watoto na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa watoto hao.
Mwilu ameelezea umuhimu wa idara hiyo kuwa na ujasiri na ubunifu katika utekelezaji wa vifungu vya sheria ili viweze kutoa ulinzi wa kweli kwa watoto.
Kulingana naye, Majaji na Mahakimu wana mamlaka ya kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa watoto walio hatarini humu nchini.
“Kila hukumu tunayoitoa, kila kesi tunayoshughulikia, ni fursa ya kupinda mizani ya haki kuelekea mabadiliko katika jamii,” alisema Naibu Jaji Mkuu huyo.
“Mapambano ya kuangamiza ajira ya watoto na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa watoto yanahusu kurejesha heshima kwa wale walio hatarini zaidi, kulinda wasiokuwa na nguvu, na kuhakikisha kuwa kila mtoto ana fursa ya kusoma, kukua na kuwa na ndoto.”
Mwilu aliyasema hayo wakati alipofunga Kongamano la Kila Mwaka la Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Strathmore jijini Nairobi.
Alipongeza kongamano hilo akilitaja kuwa jukwaa la kuakisi, kujifunza na kuchukua hatua katika kukabiliana na suala la ajira ya watoto.