Mwili wa mwanamuziki mkongwe wa Uganda Moses Matovu, utazikwa kesho Ijumaa Septemba 25, 2026, huko Kyanja, kulingana na ratiba iliyotolewa na familia yake.
Mazishi hayo ya kesho yanatangulizwa leo na maombi almaarufu Swalat Janaza katika msikiti wa Kibuli saa kumi alasiri.
Baadaye kutakuwa na mkutano wa kumkumbuka nyota huyo mwanzilishi mwenza wa bendi ya Afrigo katika ukumbi wa maonyesho ya sanaa jijini Kampala, kuanzia saa moja.
Nyumbani kwa mwendazake huo Kyanja, mkesha utaanza saa tatu usiku wa leo.
Moses Matovu au ukipenda Papa Moi alifariki alfajiri ya leo akiwa na umri wa miaka 77, kufuatia kile kilichotajwa kuwa kushambuliwa na watu wasiojulikana katika eneo la B la soko la Kibuli.
Kulingana na maafisa wa polisi, msanii huyo alikuwa akielekea msikitini kwa ajili ya maombi alipovamiwa. Alikimbizwa katika hospitali ya Kibuli lakini akaaga dunia kutokana na majeraha.
Uchunguzi wa mauaji ulifunguliwa na maafisa wa polisi huku mwana wa mwendazake aitwaye Adam Bukenya, akielezea kwamba alipata mawasiliano kunako saa kumi na dakika 45 alfajiri kwamba babake amevamiwa, akaanguka akafa.
Maafisa wa upelelezi walizuru eneo la tukio ambapo walikusanya ushahidi.
Mazingira ya shambulizi hilo hayajabainika wazi, likiwemo kusudi na utambuzi wa wahusika.