Mudavadi awaomboleza waliofariki kwenye ajali barabara ya Kitale-Webuye

Martin Mwanje
2 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametuma risala za rambirambi kwa familia za waliofariki katika ajali kwenye barabara kuu ya Kitale-Webuye katika kaunti ya Bungoma jana Jumatatu usiku. 

“Vifo vya watu zaidi ya 15 katika ajali moja ni ukumbusho wenye uchungu wa madhara yanayosababishwa na ajali barabarani,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

“Tunapoomboleza na familia zilizoathiriwa, natoa wito kwa madereva kuchukua tahadhari kubwa kwenye barabara zetu, hasa msimu huu wa mvua na nyakati zote.”

Mkuu huyo wa Mawaziri pia ameitaka Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu nchini, KENHA kutambua haraka maeneo hatari kwenye barabara kuu, na kuweka alama zinazoonekana vizuri na wakati huohuo kuimarisha uhamasisho wa usalama barabarani.

Aidha, ameitaka Mamlaka ya Kudhibiti Usalama Barabarani nchini, NTSA na polisi wa trafiki kufanya kazi kwa karibu kuhakikisha utekelezaji sheria na uondoaji wa magari yasiyostahili barabarani.

Ajali iliyosababisha kuangamia kwa watu wasipungua 15 kwenye barabara kuu ya Kitale-Webuye inadaiwa kusababishwa na dereva wa lori la masafa marefu ambaye alipoteza mwelekeo na kugonga magari kadhaa pamoja na wapita njia.

Akithibitisha ajali hiyo, kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Webuye Magharibi Rogers Bosire, alisema awali ajali ilitokea iliyohusisha pikipiki mbili na wakati umati ulipokusanyika kwenye eneo la ajali, dereva wa lori alipoteza mwelekeo na kugonga umati huo pamoja na magari yaliyokuwepo.

Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya kaunti ya Webuye kwa matibabu huku miili ya  waliofariki  ikipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo ikisubiri kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi.

Madereva wametakiwa kuwa waangalifu barabarani, hasa wakati huu wa msimu wa mvua ambapo barabara nyingi ni telezi.

Share This Article