Mudavadi ahimiza wadau wa mipango ya miji kuangazia utekelezaji wa maazimio

Alikuwa akizungumza katika awamu ya pili ya kongamano la miji barani Afrika lililoandaliwa jijini Nairobi

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi, amehimiza wadau wa mipango ya miji kuangazia utekelezaji wa maazimio.

Alikuwa akizungumza katika awamu ya pili ya kongamano la miji barani Afrika lililoandaliwa jijini Nairobi ambapo alisema, “muda wa mazungumzo umekwisha na sasa ni wakati wa vitendo.”

Mudavadi, ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka kukabiliana na kasi ya ukuaji wa miji barani Afrika, akionya kwamba kuendelea na mazungumzo bila utekelezaji kunaweza kuzidisha changamoto zilizopo.

Aliwahimiza watunga sera na wadau kubadili mwelekeo kutoka kwa majadiliano hadi kwenye miradi halisi yenye uwezo wa kufadhiliwa ambayo itaunda mustakabali wa miji ya bara hili.

Alibainisha kuwa idadi ya watu wanaoishi mijini Afrika inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 700 hadi bilioni 1.4 kufikia mwaka 2050, hali itakayoongeza shinikizo kubwa kwa makazi, miundombinu na huduma za umma.

Mudavadi alionya kuwa ukuaji wa miji usiodhibitiwa unaweza kuongeza uhaba wa makazi, uchafuzi wa mazingira na hatari za mabadiliko ya tabianchi, hali inayochangiwa na udhaifu wa mifumo ya utawala na ukosefu wa rasilimali za kifedha.

Alisisitiza umuhimu wa mipango ya kimkakati, mbinu bunifu za ufadhili na taasisi imara ili kufanikisha maendeleo endelevu.

Akitoa mfano wa Kenya, Mudavadi alieleza changamoto zilizokumba utekelezaji wa mpango wa makazi nafuu chini ya Rais William Ruto, akibainisha kuwa maamuzi ya kijasiri na wakati mwingine yasiyopendwa yalihitajika ili kusukuma maendeleo.

Alisisitiza kuwa miji iliyopangwa vyema inaweza kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, uundaji wa ajira na uendelezaji wa viwanda, huku sekta ya makazi ikiwa na nafasi muhimu katika kuchochea uchumi na kuimarisha jamii.

Mudavadi alitoa wito wa kuwa na miji jumuishi, imara na inayosimamiwa kwa ufanisi, akihimiza mataifa ya Afrika kuchukulia ukuaji wa miji kama fursa badala ya tatizo.

Alihitimisha kwa kuwataka wadau kuhakikisha kongamano hilo linazaa matokeo yenye kupimika yatakayobadilisha mustakabali wa miji ya Afrika.

Share This Article